Wizara ya Afya ya Kenya na Shirika la Afya Duniani (WHO) wanashirikiana katika mpango wa siku kumi wa mafunzo ya kukabiliana na milipuko ya kipindupindu katika kambi za wakimbizi.
Katika taarifa iliyotolewa mjini Nairobi, Kenya, Wizara ya Afya ilisema mpango huo, unaotekelezwa katika kambi za wakimbizi katika kaunti ndogo za Dadaab na Fafi mashariki mwa Kenya, unalenga watumishi wa afya, watu wa afya wanaojitolea katika jamii na viongozi wa kambi.
Kambi za wakimbizi zilizotambuliwa kama maeneo yenye ugonjwa wa kipindupindu nchini Kenya zimeshuhudia kesi 2,700 za maambukizi ya kipindupindu tangu Oktoba 2022, na kufanya iwe muhimu kwa watumishi wa afya kuongeza ujuzi na ustadi wao katika kudhibiti wagonjwa wa kipindupindu.
Mafunzo haya yanahusu masuala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na utambuzi wa mgonjwa, usimamizi wa mgonjwa katika kliniki, udhibiti wa maambukizi, mawasiliano ya hatari, ushiriki wa jamii, upimaji wa maabara, lishe na upimaji wa ubora wa maji.
Wizara hiyo ilizindua kampeni ya chanjo ya kipindupindu mapema mwaka huu, ikilenga watu milioni 2.2 wenye umri wa mwaka mmoja na zaidi.