Kiongozi wa Azimio La Umoja-One Kenya Raila Odinga amesema maandamano yanayoendelea kote nchini yanafikisha ujumbe kwa utawala wa serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Rais William Ruto.
Akiwahutubia wanahabari katika ukumbi wa Jaramogi Oginga Odinga Foundation (JOOF) jijini Nairobi mnamo Jumatano,Odinga amesema Wakenya wengi wamelemewa na gharama ya juu ya maisha.
Kinara huyo amedai kwamba jana Jumanne usiku Azimio walipata dokezi za kuwepo kwa njama ya Kenya Kwanza kukomboa wakora kuwapiga risasi viongozi ambao wangejitokeza katika uwanja wa Kamukunji huku wakora hao wakilindwa na maafisa wa polisi.
Waandalizi wa maandamano wanatoa wito wa kufutwa kwa sheria mpya ambayo inaongeza maradufu ushuru wa mafuta na kuweka ushuru wa nyumba wa 1.5% kwa wafanyikazi. Kwa sasa imesitishwa na mahakama kuu jijini Nairobi, kwa sababu ya masuala ya kikatiba.
Lakini serikali inasema hatua hiyo ni muhimu kurekebisha masuala ya ulipaji wa deni na kuunda nafasi za kazi kwa vijana wasio na ajira.
vyombo vya habari mbalimbali nchini Kenya vimeripoti mauaji ya watu sita waliopoteza maisha katika maandamano yaliyofanyika Mlolongo, kaunti ya Machakos na Kitengela, Kajiado huku baadhi ya miundo mbinu ikiwemo barabara zimeharibiwa.
Watu watatu waliuawa kwa kupigwa risasi katika mji wa Kitengela na mtu mmoja alipigwa risasi huko Emali na wawili waliuawa huko Mlolongo.