Muungano wa upinzani nchini Kenya, hivi leo unatarajiwa kufanya maandamano zaidi kupinga kile unasema kupanda kwa gharama za maisha pamoja na kuongezwa kwa kodi zinazoumiza wananchi, maandamano ambayo hata hivyo yamezuiwa na polisi.
Polisi wanasema takriban maafisa watano walijeruhiwa katika maandamano ya saba saba siku Ijumaa jijini Nairobi.
Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki alithibitisha polisi kuwapiga risasi na kuwaua watu sita katika maandamano hayo.
Maeneo mbalimbali jijini Nairobi yalionekana kuwa tulivu licha ya uwepo mkubwa wa maofisa wa polisi wa kupambana na ghasia.
Tofauti na maandamano ya awali, upinzani umeonekana kubali mkondo ambapo kwa sasa yanafanyika katika maeneo ya mikoa suala ambalo mrengo huo unasema linalenga kuwahusisha raia kutoka maeneo tofauti.
Hatua ya polisi ilipazwa sauti na rais William Ruto, ambaye amesisitiza kutokubali watu wachache waharibu amani ya nchi.
‘‘Wale ambao muko na maamuzi mahali ambapo mpo mjuwe yakwamba hamuwezi kuharibu ajira ya wakenya milioni moja.’’ alisema rais Ruto.
“Siku ya Jumatano, mtu yeyote anayetishia kufanya nchi isitawalike kupitia ghasia, uporaji, machafuko na umwagaji damu atashughulikiwa vilivyo, kwa mujibu wa sheria,” alisemaWaziri Kindiki
Mamlaka Huru ya Uangalizi wa Polisi(IPOA) inasema inachunguza visa vya ufyatuaji risasi na polisi kwa waandamanaji ambavyo viliripotiwa.
Zaidi ya watu 100 walikamatwa katika maandamano ya nchi nzima. Baadaye mahakama iliwaachilia.