Mahakama kuu nchini Kenya, imemwachia kwa dhamana seneta wa kaunti ya Uasin Gishu na gavana wa zamani Jackson Mandago na maofisa wengine wawili wanaohusishwa na sakata la ubadhilifu wa fedha za ufadhili wa wanafunzi nchini Finland unaofikia shilingi za Kenya Bilioni 1.1
Watatu hao walikamatwa siku ya Jumatano ya wiki hii kwa tuhuma za matumizi mabaya ya pesa zilizochangishwa na wazazi wa wanafunzi waliokuwa na lengo la kuwapeleka watoto wao kusomea nchini Finland na Canada.
Seneta Mandago na watuhumiwa wenzake wanatarajiwa kufunguliwa mashtaka kumi na moja kuhusiana na sakata hilo madai na tuhuma ambazo amekuwa akijitenga nazo haswa kuhusu suala la ufujaji wa fedha.
Katika taarifa ya polisi nchini humo kupitia ukurasa wa X, zamani ikijulikana kama twitter walisema mmoja wa washukiwa katika sakata hilo, Joseph Maritim, alikuwa ametoroka nchini humo.
Hata hivyo, wakili wake Maritim, Zephania Yego, ameiambia mahakama kwamba mteja wake hakuwa na ufahamu kuhusu mashtaka hao aliposafiri kuelekea nchini Canada mnamo Agosti 13, lakini atarejea kujibu mashtaka.
Upande wa mashtaka unapanga kukata rufaa dhidi ya kuachiliwa kwa seneta huyo na mshukiwa mwenzake, wakati huu Jaji akisema kesi hiyo itarejelewa baada ya mshukiwa mwingine kurejea nchini.