Kinara wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga, amesema maandamano yaliyopangwa kufanyika Jumanne ya wiki hii yatafanyika licha ya makataa ya idara ya polisi nchini humo.
Kauli yake ni wazi imelenga kuwahamasisha wafuasi wake kujitokeza barabarani hapo kesho licha ya kuwa tayari jeshi la polisi limepiga marufuku maandamano aliyoitisha
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Odinga amesisitiza kile alichosema ni serikali kutaka kuwafunga mdomo raia huku nchi ikipitia changamoto zinazohitaji kushughulikiwa haraka, ikiwemo masuala ya rushwa, ukabila, gharama ya maisha na kuibuka kwa makanisha yenye utata.
Aidha kauli ya polisi ilipazwa na kiongozi wa nchi rais William Ruto, ambaye amesema Serikali yake haitawavumilia watu ambao wanataka kuharibu uchumi za nchi hiyo kwa kufanya vurugu, akiahidi waandamanaji kukabiliwa vilivyo na mkono wa sheria.
Polisi wanasema kuwa maandamano ya awali yalisababisha vifo vya raia pamoja na kushuhudiwa kwa uharibifu wa mali ya raia, biashara zikitatizika wakati wa maandamano hayo.
Maandamano haya yanaenda kufanyika huku kamati za wabunge kutoka pande zinazozozana, wakiendelea kuvutana, kitendo kinachodhihirisha kuwa huenda kusipatikane muafaka licha ya mwito wa rais Ruto na Odinga mwenyewe.
Wito umeendelea kutolewa kwa Odinga na rais Ruto kuketi katika meza ya mazungumzo kutafuta suluhu za changamoto zao ilikuepusha kulitumbukiza taifa hilo la Afrika mashariki katika machafuko ya kisiasa.