Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Serikali cha Meru nchini Kenya, kimevumbua mfumo wa kidigitali unaofahamika kama ‘CovIdent’ utakaotoa alama za data binafsi kwa lengo la kurahisisha upimaji wa Virusi vya Corona kwa watu wengi.
Uvumbuzi huo umefanywa na Wahandisi vijana Chuoni hapo wanaotambulika kama NaiTech, chini ya usimamizi wa mhandisi Bundi Kotonya.
Mfumo wa CovIdent unaweza kutambua mtandao wa watu ambao mtu amekutana nao na hivyo kutambua wagonjwa na watu wenye uwezekano wa kuambukizwa virusi vya corona baada tu kukutana na mtu mwenye maambukizi.
Mfumo huu utasaidia kuwatambua na kuwachuja wenye maambukizi ya virusi vya corona na hivyo kupunguza kuenea kwa Covid-19 ambapo baada ya mtu kufanyiwa vipimo vya corona mfumo utaweka alama maalumu ya siri (code) na kutuma maelezo yake katika kituo cha taifa cha udhibiti wa corona au ugonjwa mwingine ambapo maelezo hayo yatahifadhiwa.
CovIdent pia utasaidia kuwapa watu nafasi ya kupata, kunakili na kutumia matokea ya upimaji wao kwa njia rahisi.
”Alama yako ya kidigitali unaweza kuitumia popote kuonyesha hali yako ya kiafya kuhusiana na corona”, amesema Profesa Romanus Odhiambo, aliyeongoza mpango wa uvumbuzi wa CovIdent na kuongeza kuwa unapotaka kwa mfano kuitumia kazini au mahala pengine unapohitajika kutambulisha afya yako kuhusu corona mfumo wa CovIdent utakutambulisha kwa njia ya alama ya siri.