Taifa la Kenya leo linaadhimisha miaka 60 ya kujitawala baada ya miongo kadhaa ya mapambano yaliyopelekea kujinyakulia uhuru na kutimuliwa mkoloni Muingereza nchini humo mwaka 1963.
Idadi ya watu wa Kenya wakati wa Uhuru ilikuwa milioni 8.6 tu. Leo, idadi ya watu inakadiriwa kuwa karibu milioni 53.
Miaka 60 tangu kupata uhuru, Kenya sio tu kwamba inasherehekea historia yake tajiri bali pia hatua muhimu zilizopigwa katika sekta mbali mbali nchini humo.
Marais watano wameongoza meli ya Kenya katika hatua tofauti za maendeleo ya taifa, kila mmoja akikabiliwa na hali tofauti ambazo zinasalia kubadilika kadri muda unavyosonga.
Pamoja na kuwa Kenya imepiga hatua kubwa za maendeleo, lakini Wakenya wanaadhimisha miaka 60 ya uhuru huku wakiwa na changamoto kama gharama za maisha kupanda, ukosefu wa ajira na majanga ya kimaumbile hasa mafuriko ambayo yanaikumba nchi hiyo hivi sasa
Rais William Ruto anatazamiwa kubainisha mafanikio ya Kenya katika miaka 60 ya uhuru na hatua ambazo serikali yake inachukua kutatua changamoto wanazokumbana nazo Wakenya.