Serikali ya Kenya inasema imeanza kuwafunza lugha ya Kifaransa maafisa wa polisi wanaotarajiwa kwenda nchini Haiti, kwenda kusaidia kukabiliana na utovu wa usalama na kuyakabili magenge ya uhalifu katika taifa hilo la Amerika Kaskazini.
Kenya inatarajiwa kutuma kikosi cha polisi zaidi ya Elfu Moja na kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya nje, Alfred Mutua, maandalizi yapo kwenye hatua za mwisho.
Wiki hii, Kenya na Marekani zimetiliana saini makubaliano ya ulinzi yatakayohakikisha taifa hilo la Afrika Mashariki linapata rasilimali na usaidizi kushugulikia vikosi vyake vitakavyotumwa nchini Haiti. Marekani imeahidi kutoa Dola Milioni 100 kuisaidia Kenya kwenye operesheni hiyo.
“Maandalizi kwa upande wetu yameshaanza, tumeshaanza kutoa mafunzo kwa maofisa wetu wa polisi iliwajifunze lugha ya kifaransa iliwapate wepesi wa kuwasiliana watakapofika huko.” alisema waziri Alfred Mutua.
Kenya inasema inauhakika kuwa hatua yake ya kuwatuma polisi nchini kufikia mwezi Januari, itamaliza magenge ambayo yamekuwa yakiwasumbua raia kwenye taifa hilo.
Mwaka uliopita, serikali ya Haiti iliomba msaada wa kimataifa kutokana na kuendelea kudorora kwa usalama unaosababishwa na makundi ya watu wenye silaha.