Wafuasi wa Chama cha Azimio la Umoja kinachoongozwa na Raila Odinga wameendelea na maandamano asubuhi hii kama walivyotangaza licha ya Rais wa Kenya William Ruto kusema yupo tayari kutumia Mamlaka aliyonayo kama Amiri Jeshi Mkuu kuzuia maandamano hayo.
Miongoni mwa matukio yaliyoshuhudiwa asubuhi hii ni kuchomwa kwa basi na matairi Barabarani, itakumbukwa juzi Ruto alisema amejaribu kuwaambia Odinga na Wafuasi wake wasiandamane ila wamekataa hivyo akaahidi kwamba wakilazimisha kuandamana watajua hawajui.
Akiongea akiwa eneo la Malava Kaunti ya Kakamega, Ruto alinukuliwa akisema “Nilimuita Odinga nikamuomba asitishe maandamano, wamekataa, Mimi niliwaambia ile wiki nyingine, nikaita yule Mzee wa kitendawili na nikamwambia wewe wacha hii maandamano tupeleke hii maneno yote unasema Bungeni, Wabunge waangalie kama kuna maneno ya ukweli”
“Sasa eti wamekataa hiyo ya kwenda kuongea kwa amani Bungeni, eti wanataka kurudia maandamano, eti waende wavunje mali na kuharibu biashara ya Wananchi, Mimi ndio commander-in-chief, nyinyi mtajua hamjui, waache hiyo mchezo”
Licha ya hayo, hali ya kawaida imeshuhudiwa katikati mwa jiji kuu la Nairobi japokuwa maeneo mengi ya biashara yamesalia kufungwa baadhi wakihofiwa kuwa huenda biahsara zao zikaporwa wakati wa maandamano hayo.
Idadi kubwa ya maofisa wa polisi pia imeshuhudiwa katika majengo ya tume ya uchaguzi IEBC, na majengo mengine ya serikali yaliokatikati mwa jiji kuu ambayo upinzani katika taarifa yake ulisema utazuru kupeleka lalama zao kwa wahusika.
Katika barabara ya Ngong, nje na jiji kuu la Nairobi, basi la abiria limeripotiwa kuchomwa moto kwa mujibu wa picha zilizochapishwa na vyombo vya habari vya ndani, watu waliokuwa wanataka kuaandamana wakidaiwa kuhusika na tukio hilo.
Maandamano ya leo Jumanne yanakuja wakati huu mkuu wa polisi jijini Nairobi Adamson Bungeiakiwa ameyaharamisha kwa msingi kuwa maandamano ya awali yaligeuka kuwa vurugu.
Licha ya polisi kukataa kutoa kibali cha kufanyika kwa maandamano hayo ya upinzani, Kinara wa Azimio la Umoja, Raila Odinga amesisitiza kuwa yatafanyika kama ilivyopangwa.