Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeidhinisha mkopo wa dola za Marekani milioni 110.5 kwa Kenya ili kuimarisha upatikanaji wa umeme kwenye nyumba za watu, miundombinu ya kijamii na biashara ndogo ndogo.
Benki hiyo imesema mkopo huo uliotengwa kwa ajili ya awamu ya tatu ya mradi wa Last Mile Connectivity, utaendeleza mpango wa serikali wa kumpatia kila mkenya huduma ya umeme.
Mkurugenzi mkuu wa AfDB katika eneo la Afrika Mashariki, Nnenna Nwabufo, amesema mkopo huo utasaidia kuendeleza miundombinu ya kijamii ya familia na wafanyabiashara wa ndani kupata umeme wa kutosha, wa kuaminika na wa bei nafuu, na kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kutimiza Ruwaza ya Kenya ya 2030.
Kwa mujibu wa takwimu za AfDB, hadi kufikia Juni 2022 takriban asilimia 77 ya wakazi wa Kenya walikuwa na umeme wa gridi ya taifa, takwimu ambazo ni zaidi ya wastani wa asilimia 50 katika eneo la Afrika kusini mwa Sahara.