Wizara ya Afya ya Kenya imezindua mkakati wa kuondoa matishio matatu ya UKIMWI, mimba za utotoni na unyanyasaji wa kijinsia ambao umerudisha nyuma maendeleo ya kufikia malengo ya Umoja wa Mataifa wa mwaka 2030.
Waziri wa afya wa Kenya Bibi Susan Nakhumicha amesema Kenya ina watu milioni 1.5 wanaoishi na HIV na zaidi ya asilimia 90 wanatumia dawa za kuokoa maisha. Alishutumu kiwango cha juu cha maambukizi kati ya vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24.
Bibi Nakhumicha amesisitiza dhamira ya serikali ya kukomesha UKIMWI ifikapo mwaka 2030 kwa kuzuia maambukizi mapya, miongoni mwa watu walio katika hatari kubwa kama vile vijana na wanawake, sambamba na kupanua upatikanaji wa matibabu ya kurefusha maisha.