Jaji Mkuu nchini Kenya, Martha Koome amesema mahakama imemwandikia barua rais William Ruto, barua ambayo inamtaka mkuu wa nchi kujadili na uongozi wa idara hiyo kuhusu madai aliyoyatoa dhidi ya baadhi ya majaji.
Rais Ruto katika siku za hivi karibuni, ameonekana kuishambulia idara ya mahakama kwa kile anachosema kuwa baadhi ya majaji ni wafisadi na wanashirikiana na upinzani kuhujumu miradi ya serikali yake.
Akizungumza na vyombo vya habari kwenye taifa hilo la Afrika Mashariki siku ya Jumatatu, jaji mkuu Martha Koome alieleza kuwa hatua ya kushambuliwa kwa idara ya mahakama na wanasiasa inaelekeza nchi hiyo katika njia mbaya na mzozo wa kikatiba.
Naye kinara upinzani kwenye taifa hilo la Afrika Mashariki Raila Odinga, amemtuhumu rais Ruto kwa kujaribu kuwatisha majaji.
Chama cha mawakili kiliandaa maandamano wiki iliyopita kulaani kile walichosema ni hatua ya mkuu wa nchi kuishambulia idara ya mahakama.