Mahakama Kuu ya Tanzania Masijala ya Kivukoni imeahirisha shauri la kikatiba la Uraia pacha hadi Mei 2,2023 ambapo pia yatajadiliwa mapingamizi ya Serikali juu ya shauri hilo ambalo lilifunguliwa December 2022 na Raia sita wa Canada, Marekani na Uingereza wenye asili ya Tanzania.
Kuahirishwa kwa kesi hiyo namba 18 ya mwaka 2022 ni kutokana na Mwenyekiti wa Jopo la Majaji watatu, Jaji Mustafa Ismail kuwa na majukumu mengine ya kiofisi ambapo hata hivyo leo upande wa Jamhuri umewasilisha takribani mapingamizi matatu ukipinga mchakato wa kufunguliwa kwa shauri hilo.
Nje ya viunga vya Mahakama, Wakili wa Wanadiaspora hao Peter Kibatala amezungumza yafuatayo “Shauri limeahirishwa hadi Mei 2 2023 ili kujadili mapingamizi matatu ya kisheria ambayo yameletwa na Serikali wakipinga kesi, kesi kama hizi haziwezi kupita bila mapingamizi hivyo ni mchakato wa kawaida, wamejibu wenzetu hoja za hawa Diaspora pamoja na hoja zao pia wameweka mapingamizi ya mchakato wa kisheria”.
Kesi hiyo imefunguliwa na Shaban Fundi, Patrick Nyelesa Nhigula, Restuta Kelemera, Njole Muya, Emmanuel Emmanuel na Bashir Kassam dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ambapo wanaiomba Mahakama itamke kuwa vifungu vya sheria ya Uraia vinavyozuia Uraia pacha ni batili wakidai kuwa vinakiuka haki zao za kikatiba kwa kuwa vinawanyang’anya haki ya asili isiyonyang’anyika kwa maana ya Uraia wa kuzaliwa.