Watu hao 65 walishtakiwa kwa kosa la kukataa kula na kunywa kwa nia ya kujiua walipokuwa wanapokea matibabu. na kesi yao inasikilizwa katika mahakama ya Shanzu kwenye mji wa Mombasa.
Zaidi ya washukiwa 10 wanaozuiliwa ikiwa ni pamoja na mhubiri anayetuhumiwa kuwashawishi mamia ya wafuasi wake kufunga kula na kunywa Paul Mackenzie walikuwa wanashindwa kutembea wenyewe kufika mahakamani baada ya kugoma kula wakiwa rumande kwa zaidi ya wiki moja.
Kesi hiyo inasikilizwa wakati idadi ya miili ya watu iliyofukuliwa kwenye msitu wa Shakahola imefika 318 baada ya miili mingine 15 kufukuliwa hapo jana.
Huku hayo yakijiri mawakili wawili wa mhubiri Mackenzie wamejiondoa kuisimamia kesi yake wakiilaumu serikali kwa kuifanya kazi yao kuwa ngumu kwa kutowapa nafasi ya kuwasiliana na mteja wao na washukiwa wengine waliokamatwa.
Wakati njaa inaonekana kuwa sababu kuu ya vifo, baadhi ya wahanga ikiwa ni pamoja na watoto walinyongwa, kupigwa au kukoseshwa pumzi, kulingana na uchunguzi wa maiti uliyofanywa na serikali.
Mackenzie dereva wa teksi-aliyegeuka-mhubiri bado hajahitajika kukiri au kukana makosa, huku upande wa mashtaka ukitaka aendelee kuwekwa kizuizini akisubiri uchunguzi zaidi.