Ni muendelezo wa kesi ya mauaji ya mtoto Asimwe Novart aliyekuwa na ualbino ambaye alichukuliwa nyumbani kwao Kamachumu may 30,2024 na June 17,2024 mwili wake ulikutwa kwenye kalavati akiwa ameuawa na kukatwa baadhi ya viungo vyake.
Washitakiwa hao tisa leo October 25 wamefikishwa Mahakama Kuu kanda ya Bukoba kwa mara ya kwanza kwa ajili ya kusomewa mashitaka yao na maelezo ya awali baada ya mwenendo kabidhi kukamilika.
Baada ya kufikishwa mahakamani hapo mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu kanda ya Bukoba Emmanuel Ngigwana,Wakili Msomi Projestus Mulokozi aliyeteuliwa na Serikali kwa ajili ya kuwatetea watuhumiwa akisaidiana na mawakili wengine wawili ameiomba mahakama kusitisha kwa muda kuwasomea mashtaka yao huku akiiomba mahakama hiyo itoe kibali kwa mujibu wa sheria dhidi ya mtuhumiwa namba moja Padri Elpidius Rwegoshora kwenda hospitalini kufanyiwa uchunguzi kwani wakati wanaongea nae wameona kama ana changamoto ya akili.
Hoja hiyo imeungwa mkoni na mawakili wenzake wa upande wa utetezi na Jamhuri,ndipo Jaji Emmanuel akaanza kumuuliza maswali mbalimbali mtuhumiwa huyo namba moja Padri Elipidius Rwegoshora “unajua kwa nini upo Mahakamani?” Akajibu “niliambiwa na RCO kuwa nimeua mtoto”
Akamuuliza tena “tangu umezaliwa uliwahi kuwa na changamoto yoyote ya kiafya upande wa akili na ukapelekwa hospitali?”
Akajibu “waga nina tatizo la kusahau na nilisimamishwa kazi eti maneno yangu sio mazuri”.
Baada ya maelezo hayo Jaji amesema kuwa Mahakama inaona hawawezi kuendelea na watuhumiwa hao wengine nane badala yake ametoa siku 42 kwa mtuhumiwa huyo namba moja Elipidius Rwegoshora kupelekwa Isanga taasisi ya akili kwa ajili ya uchunguzi.
Washtakiwa hao tisa kwenye kesi namba 25513 ya mwaka 2024 ni Elipidius Rwegoshora ambaye ni padri, Novat Venant ambaye ni baba wa mtoto Asimwe, Nurdin Ahmada, Ramadhan Selestine, Rwenyagira Alphonce, Dastan Buchard, Faswiu Athuman, Gozibert Arikad na Dezdery Everigist ambapo washitakiwa nane wamerudishwa rumande mpaka Desemba 11 mwaka huu 2024 huku Elipidius Rwegoshora akipelekwa Isanga.