Kesi inayomkabili aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na wenzake imeshindwa kuendelea baada ya Upande wa Mashtaka kushindwa kuwasilisha jalada wakati kesi hiyo.
Mahakama hiyo, ilitarajia kusikiliza maombi yaliyowasilishwa na wadhamini wa mshitakiwa huyo wakiomba mahakama kutoa hati ya kumkamata mshitakiwa huyo kwa kuwa wao wameshindwa.
Wakili wa Serikali, Ester Martin amemueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa mwendesha mashitaka anayesikiliza shauri hilo hayupo hivyo anaomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kusikilizwa.
Baada ya Upande wa mashitaka kuwasilisha hoja hiyo, Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Aprili 23, 2020 kwa sababu ya Upande wa Mashitka umeshindwa kuwasilisha jalada la kesi hiyo mahakamani hapo.
Mbali na Lissu washitakiwa wengine ni Simon Mkina, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob ambapo kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka ya uchochezi.
Katika kesi ya msingi kwa pamoja washtakiwa hao, wanakabiliwa na mashtaka matano ikiwamo kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.
Ilidaiwa kuwa kati ya Januari 12 hadi 14, 2016 jijini Dar es Salaam, washtakiwa Jabir, Mkina na Lissu, waliandika na kuchapisha taarifaza uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar.’
Katika shtaka la pili wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.
Mshtakiwa Mehboob anadaiwa kuwa Januari 13 ,2016 katika jengo la Jamana lililopo Manispaa ya Ilala, alichapisha gazeti la Mawio lililokuwa na taarifa za uchochezi.
Ilidaiwa kuwa mshtakiwa huyo pia alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.