Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Angellah Kairuki amesema amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Dkt. Isaack Daniel Athumani Sima aliyekuwa Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Nyamongo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Mkoani Mara.
Kifo cha Dkt. Isaack kimetokea usiku wa tarehe 03.05.2023 wakati akitoka nyumbani kwake kuelekea kwenye kituo chake cha kazi kwa kupigwa nondo na Watu wasiojulikana hadi mauti kumfika.
Kairuki ametoa pole kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Familia, Ndugu, Jamaa na Marafiki kwa msiba huo.
Kufuatia tukio hilo la kusikitisha ambalo limetokea wakati Mtumishi wa umma akienda kutekeleza majukumu yake, Kairuki ameomba Vyombo vya Ulinzi na Usalama kuchunguza tukio hili kikamilifu na kuwachukulia hatua wale wote watakaobainika kuhusika na tukio hilo.