Moja ya habari iliyo washangaza wengi ni hii ya kijana mmoja mkazi wa Moscow hivi majuzi alipigwa faini na kufunguliwa mashtaka na polisi kwa kupaka nywele zake rangi ya njano na bluu, rangi za bendera ya Ukraine.
Usiku wa Aprili 27, Stanislav Netesov alishambuliwa na washambuliaji wasiojulikana kwenye kituo cha basi katikati mwa Moscow alipokuwa akirejea kutoka kazini.
Aliibiwa simu na jino kung’olewa, lakini alipokwenda Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi katika wilaya ya Tverskoy siku iliyofuata kuripoti uhalifu huo alishtuka kujua kwamba badala ya kumpa msaada, wenye mamlaka walimuweka rumande kisa rangi ya nywele zake.
Netesov alikuwa na nywele zake zilizotiwa rangi ya manjano, bluu na kijani, jambo ambalo polisi waliliona kuwa ishara ya Ukrainia na kosa kwa jeshi , ambalo linaadhibiwa kisheria.
Stanislav Netesov alisema kwamba polisi walitoa ripoti juu yake kwa “uhalifu” wake, walichukua alama za vidole vyake, na kumpa hati ya wito kwa ofisi ya usajili wa kijeshi na uandikishaji, wakitangaza kwamba watamlazimisha “kubusu ardhi yake ya asili kwenye mitaro. ”
Mahakama za Urusi zinatambua taarifa zozote zinazochukuliwa kuwa za kupinga vita kuwa za kudharau jeshi, uhalifu unaoweza kuadhibiwa kwa faini ya hadi rubles 50,000 ($543), na kifungo cha hadi miaka mitano jela kwa makosa yanayorudiwa mara kwa mara.