Utafiti wa Madaktari wa Idara ya Magonjwa ya Mfumo wa Mkojo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa umebainisha kuwa mitindo mbalimbali ya kujamiiana inaweza kusababisha uume uliosimama kwa muda mrefu kuvunjika ukiwemo mtindo wa Mwanaume kukaliwa juu na Mwanamke mwenye uzito mkubwa.
Utafiti wa Madaktari hao umechapishwa kwenye Jarida la kimataifa la Case za Upasuaji (International Journal of Surgery Case Reports, 108(2023)108415) ambapo wameripoti kufanya upasuaji wa kuunga uume wa Kijana mwenye umri wa miaka 27 uliovunjika wakati akijamiana na Mkewe.
Kwa mujibu wa taarifa ya utafiti huo, ajali ya kuvunjika uume si suala lenye kujitokeza mara kwa mara, lina uwiano wa 1 kati ya Watu 175,000.
Hata hivyo, utafiti huo unadokeza kuwa tafiti zilizofanyika katika Mataifa ya Ulaya na Marekani zimeonesha kuwa asilimia 93.3 ya ajali za uume hutokana na kujamiiana, ambacho kilikuwa chanzo cha ajali ya uume aliyoipata Kijana aliyetibiwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa.