Idara ya polisi imetoa mwelekeo jinsi maafisa wa polisi wanaotarajiwa kwenda katika oparesheni ya kutokomeza magenge ya ujambazi nchini Haiti mapema mwakani watakavyochaguliwa.
Kwa mujibu wa agizo hilo, idara ya polisi inalenga kupeleka angalau maafisa wa polisi 1000 nchini Haiti mwezi Januari mwakani.
Agizo hilo limetolewa kwa maafisa wakuu katika kila kituo cha polisi nchini kupendekeza angalau maafisa 2 kutoka kila kituo kote nchini ili kutengeneza kikosi cha maafisa 1,000 kwenda Haiti, gazeti la The Standard limeripoti.
Wiki iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliidhinisha ujumbe wa Multinational Security Support (MSS) kwenda Haiti, kwa lengo la kutoa misaada kwa watu wa Haiti, ambao wamevumilia mateso ya muda mrefu kutokana na vitendo vya uhalifu wa kutumia nguvu.
Katika kujibu ombi la kuongoza misheni nchini Haiti, Rais William Ruto alikubali, na Kenya inatarajiwa kuchangia kikosi cha maafisa wasiopungua 1,000, pamoja na idadi isiyojulikana ya maafisa kutoka Jamaica, Bahamas, na Antigua na Barbuda.
Kulingana na mawasiliano ya siri, OCS wanaagizwa kuchagua maafisa walio na kiwango cha chini cha miaka mitano ya huduma hai katika huduma ya polisi ya kitaifa, na maafisa hawa lazima wawe na umri wa kati ya miaka 20 na 55.
Wakati huo huo, waziri wa usalama wa ndani Profesa Kithure Kindiki amewahakikishia Wakenya kwamba zoezi la kuteuliwa kwa maafisa hao kutoka kila kituo liyakapokamilika, mchakato mzima utaidhinishwa na bunge.