Rais Alexander Lukashenko wa Belarus amesema anapanga kuunda jeshi jipya la kikandarasi na kulitumia ndani yake kundi la mamluki la Wagner.
Rais wa Belarus amesisitiza kuwa nchi yake haijapanga kushiriki katika vita vyovyote na akaongeza kuwa: kuundwa kikosi kipya katika jeshi ni kwa ajili ya kuongeza nguvu na uwezo wa kiulinzi tu.
Waziri wa Ulinzi wa Belarus, Viktor Khornin alieleza hapo kabla kuwa askari wa kikandarasi na wa mkataba wanaunda karibu 60% ya jeshi la Belarus.
Wizara ya Ulinzi ya Belarus na Kamandi ya kundi la Wagner zimeandaa mpango wa kushirikiana kuanzia siku chache zijazo.
Wakufunzi na vitengo vya kundi la Wagner hivi sasa vinashiriki katika kazi za utoaji mafunzo katika jeshi la Belarus, lakini upande wa Belarus hadi sasa haujatangaza ni wanajeshi wangapi wa kundi la Wagner waliopo kwenye ardhi ya nchi hiyo.
Ikumbukwe kuwa vikosi vya Wagner vilihamishiwa Belarus mwezi uliopita baada ya uasi uliozuka dhidi ya serikali ya Russia.