RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Jakaya Mrisho Kikwete ameipa klabu ya Simba Sh 30 milioni kwa ajili ya kukomboa hati yao ya kiwanja cha Bunju B, Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage aliwaambia wanachama wa klabu hiyo jana Jumapili katika mkutano wa wanachama wa klabu hiyo uliofanyika Bwalo la Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam.
Rage alisema kwamba Rais Kikwete ametoa fedha hizo baada ya kufurahishwa na umoja ulionyeshwa na baadhi ya wanachama wa Simba waliojitolea kwenda katika uwanja huo kwa siku za karibuni na kufyeka majani na kuonyesha kuwa wanauhitaji.
Rage alisema alikutana na Rais Kikwete saa 2 asubuhi jana Jumapili kabla ya kufanyika kwa mkutano mkuu wa Simba na kumtakia heri katika mkutano huo huku pia akitoa hundi ya Sh 30 milioni kwa ajili ya uwanja huo.
“Asubuhi leo saa 2 nilipata bahati ya kukutana na Rais Kikwete na kututakia heri katika mkutano wetu na kama unavyojua kulikuwa na matatizo ya kupata hati ya ardhi kule Bunju, tulikuwa tunadaiwa Sh 85 milioni, tulitoa milioni 50 hivyo nikamuomba Rais aingilie kati jambo hili ili kuweza kupata hati mapema na kuanza ujenzi.”
“Rais akanikabidhi hundi ya milioni 30 kama mchango wake kwetu, amedhihirisha ni mwanamichezo na mpenzi wa timu zote, kutokana na jambo hilo naamini mambo yatakwenda vizuri na zile siku 100 alizotoa katibu wa Simba kuwa baadhi ya vitu vitakuwa vimekamilika basi vitakamilika kweli maana hadi kufikia siku hizo tutakuwa hata na sehemu ya kufanyia mazoezi timu yetu,” alisema Rage.
Aliongeza: “Kikubwa alichofurahishwa ni juhudi za wanachama kwenda kule na kuonyesha uhitaji wa uwanja na ndio maana akaamua kutoa fedha hizo ili kuhakikisha tunapata hati ya ardhi na kuanza ujenzi mara moja.”
SOURCE: MWANASPOTI