Upande wa utetezi katika kesi inayomkabili Ofisa Programu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadàmu LHRC Tito Magoti na mwenzake umedai habari zisizo rasmi ni kwamba mchakato wa kukiri makosa kwa washtakiwa hao umeshindikana.
Mshtakiwa mwingine kàtika kesi hiyo ni mtaalam wa masuala ya Tehama (ICT) Theodory Giyan ambapo jana hakufika mahakamani kwa madai kuwa ni mgonjwa.
Wakili wa Utetezi Jeremia Mtobesya alidai hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Janet Mtega.
Awali, Wakili wa Serikali Estar Martin alidai, kesi hiyo imeletwa kwa ajili ya kutajwa na kwamba upelelezi bado haujakamilika.
Alidai hata hivyo, washtakiwa walikuwa wanaendelea na mchakato wa kukiri makosa yao kwa kuingia makubaliano na ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP).
Ndipo Wakili Mtobesya alipoieleza Mahakama kuwa kweli kulikuwa na utaratibu huo unaendelea lakini habari zisizo rasmi kutoka kwa Wakili mwenzake ni kwamba mchakato huo ulishindikana.
“Tarehe ijayo tutakaa na mwenzangu hivyo tutapata msimamo kama huo mchakato ulishindikana au la, pamoja na hilo tunaomba upande wa mashtaka uharakishe upelelezi wa kesi” Mtobesya
Baada ya melezo hayo, kesi hiyo iliahirishwa hadi Novemba 24 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.
Katika kesi hiyo, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka matatu ambayo ni kuendesha genge la uhalifu, kumiliki programu ya kompyuta kwa lengo la kutenda makosa ya jinai na kutakatisha zaidi ya sh Milioni 17.
Ilidaiwa kati ya Februari mosi hadi Desemba 17 mwaka huu katika maeneo mbalimbali jijini DSM na ndani ya Jàmhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa nia ovu wakiwa na wenzao ambao hawapo Mahakamani, walishiriki genge la uhalifu na kujipatia Sh. 17,354, 535.
Shtaka la pili ilidaiwa kuwa, katika tarehe na maeneo hayo, washtakiwa hao wakiwa na wenzao ambao hawapo Mahakamani, walitenda kosa la kumiliki programu ya kompyuta iliyotengenezwa mahususi katika kutenda makosa ya jinai.
Katika shtaka la tatu la utakatishaji fedha ambapo ilidaiwa katika tarehe hizo jijini DSM, washtakiwa hao wanadaiwa kujipatia Sh. 17,354, 535 wakati wakijua fedha hizo ni mazalia ya kosa la kuendesha genge la uhalifu.