Kutokana na kuendelea kwa changamoto ya uharibifu wa vyanzo vya maji vilivyopo chini ya Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu bodi hiyo imekutana na kamati ya Ulinzi na usalama Wilaya ya Morogoro ili kuona namna ya kukabiliana na changamoto hiyo.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Maji Bonde la Wami – Ruvu Mhandisi Elibarik Mmassy amesema hali ya uharibifu wa vyanzo vya maji bado ni changamoto hivyo jitihada za haraka zinahitajika kunusuru suala hilo.
Anasema licha ya kuendelea kitoa elimu kwa wananchi bado Wananchi wamekua wakikaidi na kufanya Shughuli za kibinadamu katika vyanzo vya maji ikiwemo kilimo,ufugaji uchimbaji madini jambo ambalo linahatarisha usalama wa wananchi hasa wakati wa ukame.
Mhandisi Mmasy anasema licha ya kutoa elimu lakini pia wamejenga mabirika ya kunywesha mifugo, kugawa mizinga ya nyuki na kutoa miti rafiki ya maji ili Wananchi wanaishi karibu na vyanzo vya maji waweze kutumia shughuli za hizo na kujingizia kipato.
Kwa upande wake Afisa Tawala Wilaya ya Morogoro Hilali Sagara akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Bi. Rebecca Nsemwa amesema serikali itaendelea kushirikiana na Bosi hiyo katika Usimamizi wa sheria ili hatua zichukuliwe kwa wale wanaovunja sheria.
Nao wakazi wa Morogoro wameiomba Serikali kusimamia Sheria ili kuthibiti vyanzo hivyo kwani kinachoonekana hadi changamoto hiyo kuendelea ni viongozi wenye Mamlaka husika kushindwa kusimamia sheria na watu kuona jambo la kawaida licha ya kutambua kuwa kufanya hivyo ni kosa.
Kikao hicho ambacho kimeketi kwa zaidi ya masaa manne kimeadhimia mambo mbalimbali ambapo utekelezaji wake unaanza leo huku msisitizo ukitolewa kwa jamii inayoishi karibu na vyanzo vya maji kuheshimu na kilinda vyanzo huku wakitambua kua wao ndio tegemeo kwa Wananchi wengine.