Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (KUWASA) Manispaa ya Kigoma Ujiji imeanza utekelezaji wa mradi mkubwa wa uongezaji wa mtandao wa maji wenye urefu wa kilometa 90 ambao umewezesha zaidi ya wakazi 4,000 wa kijiji cha Kalalangabo kupata huduma ya maji safi na salama, ambayo awali iliwalazimu kutegemea maji ya Ziwa Tanganyika.
Mradi huo ambao unagharimu jumla ya shilingi bilioni 1.9, unajumuisha pia marekebisho ya baadhi ya mabomba chakavu.
Utekelezaji wa mradi huo ulianza baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji, ambao umeweka historia mpya kwa mji wa Kigoma.
Akizungumza kuhusu mradi huo, Kaimu Mkurugenzi wa KUWASA, Mhandisi Poas Kilang, amesema kuwa jitihada kubwa zinaelekezwa kwenye maeneo yenye changamoto kubwa ili kusaidia wakazi wanaopata shida kutafuta huduma ya maji.
“Mradi huu wa shilingi bilioni 1.9 ni sehemu ya juhudi zetu za kuimarisha huduma ya maji katika eneo hili, tunakusudia kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2025, asilimia 95 ya wakazi wa Kigoma Ujiji wanapata maji safi na salama.”
Kijiji cha Kalalangabo, kilichopo katika Halmashauri ya wilaya ya Kigoma, kilikuwa moja kati ya maeneo yaliyoathiriwa na ukosefu wa maji safi na salama kutokana na ukosefu wa miundombinu ya kutosha ya maji ambapo awali kulikuwa na magati kumi, lakini moja tu ndilo lilikuwa likitoa huduma ya maji, hata hivyo, juhudi za KUWASA zimeanza kuzaa matunda.
Mhandisi Fransisco Makoye, Mhandisi wa Uendeshaji wa KUWASA, amesema: “Tayari tumefikisha kilometa 45 za mtandao wa maji, na wakazi wa eneo hili sasa wanapata maji safi na salama kwa urahisi. Hatimaye, wameondokana na haja ya kutegemea maji ya Ziwa Tanganyika.”
Wakazi wa Kalalangabo akiwemo Fathuma Ibrahimu na Lewina Chamlanga wameelezea maendeleo hayo kwa kusema, Sasa wanapata u maji kwa urahisi na hayana uchafu kama maji ya ziwa lakini pia kuondokana na changamoto ya kutemba zaidi ya sa moja kufuata maji.
Rulinga Rashi Afisa mtendaji kata ya Ziwani anasema sasa wameanza kutoa fomu kwa wananchi ili kila mtu awe na bomba nyumbani kwake ili kuongeza ufanisi katika upatikanaji wa huduma hiyo muhimu.
KUWASA imesema inaendelea kufanya kazi kufikia lengo lake la kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama kwa hadi asilimia 95 kwa wakazi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji ifikapo mwaka 2025.