Rais wa Korea Kaskazini, Kim Jong-Un amekiri nchi yake kukabiliwa na baa la njaa, akisema hali ya uhaba wa chakula inazidi kuwa mbaya wakati taifa hilo likiwa katikati ya mapambano dhidi ya virusi vya corona na vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na Marekani kufuatia majaribio ya silaha za nyuklia yanayoendelea kufanywa na taifa hilo.
Akifungua Mkutano Mkuu wa Chama Cha Wafanyakazi kinachotawala nchi hiyo, Kim amewasisitiza viongozi kutafuta suluhu ya baa la njaa lililotokana na uzalishaji haba wa chakula baada ya kimbunga kilichoikumba nchi hiyo mwaka jana.
Korea Kaskazini inadaiwa kukabiliwa na uhaba wa tani milioni moja za chakula, huku bei za vyakula mitaani zikipanda kufikia mara tatu ya bei ya kawaida. Utafiti wa Kitengo cha Chakula cha Marekani unakadiria upungufu wa tani zingine milioni 1.35 za chakula mwaka huu, huku mahitaji ya chakula nchini Korea Kaskazini yakiwa tani milioni 5.75 kwa mwaka.
Korea Kaskazini inakabiliwa si tu na uhaba wa chakula, uchumi wa taifa hilo umeporomoka kwa takriban 10%, ikiwa ni mdororo mbaya zaidi tangu miaka ya 1990, huku mapambano dhidi ya virusi vya corona yakiilazimisha taifa hilo kufunga mipaka yake kwa mshirika wake mkubwa zaidi wa kibiashara, China, na kufanya hali ya biashara kuwa ngumu zaidi kutokana na vikwazo vikali vilivyowekwa na Marekani vinavyoifanya taifa hilo la Kikomunisti kushindwa kufanya biashara na mataifa mengine duniani.
Kabla ya kuzuka kwa virusi vya corona, thamani ya biashara kati ya Korea Kaskazini na China ilifikia dola bilioni 2.8 kwa mwaka, lakini kwa sasa thamani hiyo imeporomoka kufikia dola milioni 540 tu kwa mwaka, kipaumbele cha Kim kikiwa kuzuia virusi vya Corona kuingia nchini humo.