Kiongozi mkuu wa mbio za Mwenge wa uhuru Kitaifa 2023 Abdalah Shaib Kaim amesisitiza suala la utunzaji wa mazingira katika vyanzo vya maji lizingatiwe huku kuwekewa mkazo wa usimamizi wa Sheria za mazingira
Abdalah ameyasema hayo wakati wa zoezi la upandaji miti kwenye mto Lumemo kata ya Mbasa na Kibaoni halmashauri ya Ifakara Mji wilaya ya Kilombero Mkoani Morogoro ikiwa ni mwendelezo wa mbio za Mwenge mkoani humo.
Kiongozi huyo mbio za Mwenge za uhuru Kitaifa 2023 amesema licha ya kuwepo kwa sheria za utunzaji mazingira na vyanzo vya maji bado kumekuwa na changamoto ya watu kufanya shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo ,uchimbaji mchanga na ufyatuaji tofali hivyo mamlaka husika zinapaswa kusimamia sheria hizo ili kupunguza athari za uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji.
Amesema uharibifu wa mazingira unaleta athari kubwa ikiwemo mabadiliko tabia nchi na kusabisha mafuriko na ukame .
Mbunge wa jimbo la Kilombero Mheshimiwa Abubakari Asenga anasema mto huu ni miongoni mwa mito inayopelekea maji katika mto Kilombero kwa asilimia 25 ambapo mto.kilombero unachangia maji katika bwawa la Mwalimu Nyerere kwa asilimia 65
Asenga anasema mara kwa mara amekua akifanya mikutano na wananchi amekua akiwashirikisha bodi ya maji bonde la Rufiji -Kilombero ili kusaidiana kutoa elimu kwa wananchi faida za utunzaji vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla.
Awali akisoma taarifa kwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa ,afisa maji Bonde la Rufiji -Kilombero Emanueli Lawi amesema mradi huo wa wa utunzaji wa vyanzo vya maji na manzingira katika chanzo cha moto Lumemo wenye thamani ya shilingi milioni 12 malengo ya kurudisha uoto wa asili katika mito inayosimamiwa na bodi ya Maji Bonde la Rufiji -Kilombero
Anasema kwa siku ya uzinduzi wa miradi wamepanda miti zaidi ya 1500 katika mto huo wa Lumemo na mpango uliopo ni kufikia mito yote inayohifadhiwa na bodi hiyo.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kilombero Wakali Dunstan Kyobya amesema mto Lumemo umekua chanzo kikuu cha mafuriko katika mji wa Ifakara hivyo mradi huo unaleta matumani kwa kuzuia athari za uharibifu mazingira.
Anasema licha ya kupanda miti katika mto huo mpango wa serikali ni kupanda miti zaidi ya milioni moja na laki tano kwa kwa halmashauri zote za wilaya hiyo ambazo ni Ifakara Mji na Mlimba .
Nao baadhi ya wakazi wanaozunguka maeneo ya hifadhi na vyanzo vya maji wanasema wameweka utaratibu kuweka ulinzi shirikishi katika maeneo hayo ili kuwabaini watu wanaofanya uharibifu wa vyanzo vya maji.