Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema ni marufuku kwa Wakurugenzi wa Halmashauri na Watendaji mbalimbali kuchukua ardhi ya mtu kama hawana fedha ya kulipa fidia.
Pia amesema hivi karibuni Serikali itasajili madalali wote lengo likiwa ni kuondoa utapeli ambao umeendelea kuwepo kwa baadhi ya madalali ambao sio waaminifu.
Akizungumza na Watendaji wa Ardhi mkoani Dodoma, Waziri Lukuvi amepiga marufuku kwa Wakurugenzi wa Halmashauri na watendaji mbalimbali nchini kuchukua ardhi ya mtu kama hakuna fedha ya kulipa fidia.
Kikao hicho kiliandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka kwa ajili ya kusaidia kutatua migogoro ya ardhi katika Jiji la Dodoma.
“Kiongozi wa serikali hawezi kuwa mwizi, Dodoma mlikuwa mnatumia ubabe sana, ardhi ni yangu lazima tuelewane, kwenye ardhi hakuna ubabe lazima tusimamie sheria. Usiitamani ardhi ya mtu tafuta hela Mkurugenzi kama huna hela ya kulipa achana nae” Lukuvi
“Hatuwezi kuendeleza migogoro unataka kujenga Zahanati kwenye ardhi ya mtu lipa kwanza fidia ndio uendelee na ujenzi hata kwenye dini wanasema usitamani kisichochako, huna hela niachie ardhi yangu lakini fidia lazima unipe,” Lukuvi
Amesema kwa sasa serikali itasajili madalali wote ili kuondoa utapeli ambao umekuwa ukitokea katika ardhi.
“Kamateni matapeli kwa Dodoma ni wengi na wanaendelea kuwaibia watu. Sasa tunakuja na mfumo wa kusajili madalali wote na lazima awe na ABC katika ardhi kwani wengi ni wezi tu,”