Kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Bobi Wine, ameripotiwa kupigwa risasi mguuni na maafisa wa usalama katika kitongoji cha kaskazini mwa Kampala, chama chake kimesema. Wine, ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi, aliibuka kama mpinzani mkuu wa Rais Yoweri Museveni, na alimaliza wa pili katika uchaguzi wa urais wa 2021.
Chama chake, National Unity Platform (NUP), kilidai kwenye mtandao wa X kuwa maafisa wa usalama walijaribu kuondoa uhai wake, na Wine alijeruhiwa vibaya. Hata hivyo, polisi walisema kuwa walikuwa wakijaribu kumzuia Wine na timu yake kutembea barabarani, na mvutano huo ulisababisha jeraha lake.
Katika video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii, Wine alionekana akisaidiwa kutoka kituo cha afya cha Najeem huku akionyesha jeraha la damu mguuni. Chama cha NUP kililaani tukio hilo, kikisema ni jaribio lingine la kuondoa uhai wa kiongozi huyo wa upinzani, huku wakitaka jamii ya kimataifa kulaani vurugu zinazowakabili wapinzani wa Museveni.
Serikali ya Rais Museveni imekuwa ikituhumiwa kukandamiza upinzani, madai ambayo Rais huyo ameyakana. Marekani pia imeeleza wasiwasi wake juu ya hali ya demokrasia nchini Uganda, ikisema kuwa nafasi ya kidemokrasia inazidi kupungua.