Wizara ya Afya ya Zambia imetangaza kuwa, maambukizi ya ugonjwa wa Kipindupindu yamebainika katika karibu nusu ya wilaya zote za nchi hiyo na mikoa tisa kati ya 10. Kesi 400 mpya za watu walioambukizwa ugonjwa huo zinaripotiwa kila siku huku idadi ya watu waliofariki hadi sasa ikipindukia 400.
Taarifa ya wizara hiyo imeongeza kuwa, mripuko huko mkubwa wa Cholera umeshawakumba watu zaidi ya 10,000, na kusababisha mamlaka kuagiza skuli kote nchini kusalia kufungwa baada ya mapumziko ya mwisho wa mwaka.
Mripuko wa ugonjwa huo nchini Zambia ulianza mwezi Oktoba, ambapo watu 412 wameshafariki dunia hadi sasa, na kesi 10,413 zimerekodiwa. Hayo ni kulingana na hesabu za jana Jumatano zilizotolewa na Taasisi ya Afya ya Umma ya Zambia, chombo cha serikali kinachoshughulikia masuala ya dharura za kiafya.
Waziri wa Afya wa Zambia, Sylvia Masebo amesma, mripuko huo, ambao ameuelezea kuwa janga la nchi nzima, unaendelea kuwa tishio kwa usalama wa afya ya taifa.
Kwa mujibu wa Bi Masebo, kesi nyingi za maambukizi ziko katika mji mkuu Lusaka, ambapo uwanja wa taifa wa soka wenye viti 60,000 umebadilishwa kuwa kituo cha matibabu na unashughulikia wagonjwa karibu 500 kwa wakati mmoja.
Waziri wa afya wa Zambia ameongeza kuwa, nchi hiyo imepokea takribani dozi milioni 1.4 za chanjo ya kipindupindu kutoka Shirika la Afya Duniani [WHO] na wanatarajia dozi 200,000 zaidi kuwasili hivi karibuni.