Shambulio la Iran ambalo halijawahi kushuhudiwa dhidi ya Israel limeashiria mvutano mpya katika mzozo wa Mashariki ya Kati.
Iran imejitetea ikisema kuwa shambulizi hilo lilitokana na shambulizi la anga lililodaiwa kufanywa na Israel katika ofisi zake za ubalozi nchini Syria ambapo majenerali wawili pamoja na walinzi wake wa kijeshi waliuawa Aprili 1.
Hata hivyo, viongozi kadhaa wa dunia kama vile Rais wa Marekani Joe Biden, na Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak wamelaani hatua hiyo ya Iran.
Israel ilisema kuwa zaidi ya ndege 300 zisizo na rubani na makombora zilirushwa na Iran Jumamosi usiku lakini walifanikiwa kuzuia 99% yao.
Hasa, shambulio la Iran limezusha hofu zaidi ya vita huko Gaza vilivyoanza Oktoba 7, 2023, baada ya Hamas kufanya mashambulizi ya mpakani dhidi ya Israel ambayo yalisababisha vifo vya watu 1,170, wengi wao wakiwa raia.
Mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Israel yameua takriban watu 33,729 huko Gaza, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas.