Leo May 16, 2018 Upande wa utetezi katika kesi ya uchochezi inayowakabili Viongozi wa CHADEMA akiwemo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe umeiomba mahakama kuwafutia mashtaka washtakiwa kwa kuwa yana mapungufu kisheria.
Maombi hayo yamewasilishwa na Wakili wa utetezi, Peter Kibatala mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Wilbard Mashauri wakati kesi hiyo ilipoitishwa ili washtakiwa wasomewe maelezo ya awali (Ph).
Katika maombi hayo ambayo Kibatala aliwasilisha mapingamizi 8, ambapo amedai, kibali cha DPP kina upungufu wa kisheria kwa sababu haioneshi imetolewa kwa mashtaka yapi.
Pia hati ya mashtaka imewataja majina washtakiwa wote bila ya kufafanua, pia imetaja kifungu cha sheria ambacho washtakiwa wameshtakiwa nacho.
Katika pingamizi hilo, Kibatala amedai kuwa kibali kilichowasilishwa mahakamani hapo kwa maana hiyo mashtaka dhidi ya washtakiwa yamepelekwa mahakamani hapo bila ridhaa ya DPP.
Aidha Kibatala amedai kuwa, iwapo kama mahakama itashindwa kuifuta hati nzima ya mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao basi iyafutilie mbali mashtaka ambayo yana mapungufu kisheria, ikiwamo shtaka la nne, latano, la sita na la saba.
Akijibu hoja hizo, Wakili wa serikali Mkuu, Paul Kadushi aliiomba mahakama kuyatupilia mbali mapingamizi yote hayo ya upande wa utetezi kwa kuwa hayana mashiko kisheria.
Kuhusu kibali cha DPP kinachoipa mahakama ridhaa ya kusikiliza kesi hiyo, Kadushi amedai kuwa hakuna uamuzi wowote ulioweka msingi kwamba ni lazima kiwepo na nini hakipaswi kuwepo.
Mbali na Mbowe wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo Namba 112 ya 2018 ni mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu na Naibu katibu Mkuu bara na Mbunge wa kibamba John Mnyika.
Mbunge wa Tarime mjini Esterher Matiko, Katibu wa chama hicho Dr. Vicenti Mashinji na mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe Halima Mdee na mbunge wa Bunda, Esther Bulaya.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na jumla ya mashtaka 12 katika kesi ya jinai namba 112 ya mwaka 2018 ikiwamo kula njama, kufanya mkusanyiko usio halali kinyume cha sheria na kuendelea kufanya mkusanyiko usio halali ama maandamano yaliyosababisha kifo cha Akwilina.
Mahakama imetaja sababu za kumuachia aliyenasishwa kiroba cha mahindi