Meneja wa Liverpool Jurgen Klopp anatarajia kuwa nje ya kinyang’anyiro cha kuwania taji la Premier League kabla ya timu yake kuzuru Aston Villa siku ya Jumatatu, lakini ameweka lengo jipya la timu yake kufikisha pointi 80 huku wakipania kumaliza kwa nguvu.
Liverpool walio katika nafasi ya tatu walikuwa na matumaini ya kushinda taji hilo baada ya msururu wa matokeo mabaya mwezi uliopita na ingawa kihesabu bado wana nafasi, huenda isiwe hivyo watakapowasili Villa Park.
Manchester City, iliyo katika nafasi ya pili, itamenyana na Fulham kesho huku vinara wa ligi hiyo Arsenal wakicheza na Manchester United siku ya Jumapili na iwapo mojawapo ya timu mbili za juu itaambulia pointi tatu basi matumaini madogo ya Liverpool yatazimika.
Klopp, ambaye ataondoka Anfield mwishoni mwa msimu huu na atasimamia mechi yake ya mwisho ya ugenini ya Liverpool akiwa Villa, hatarajii kuteleza.
“Sote tunaweza kusoma jedwali na kuona hali ilivyo,” alisema akiwa na Liverpool yenye pointi 78, tano nyuma ya Arsenal na nne nyuma ya City ambao wana mchezo mkononi. “City inabidi wapoteze mechi tatu. Ni ngumu kuona hilo, lakini huwezi jua. Arsenal lazima wapoteze mechi mbili, ngumu. Wote wanacheza mbele yetu, kwa hiyo tuzungumze Jumatatu ikiwa wote watapoteza, lakini sitarajii hilo.
“Nadhani tunayo ya kutosha kufanya. Tunayo nafasi ya kuvuka pointi 80 tena; kama vile kila kitu maishani, kamwe usichukue mambo kama haya kuwa ya kawaida.”