Gervais Hakizimana, kocha wa mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za masafa marefu za wanaume Kelvin Kiptum, anatarajiwa kuzikwa nchini kwao Rwanda.
Wawili hao walifariki katika ajali ya gari magharibi mwa Kenya tarehe 11 Februari. Mwanafamilia wa Hakizimana aliliambia gazeti la Nation la Kenya kwamba mazishi yatafanyika saa 14:00 kwa saa za Rwanda (12:00 GMT) kwenye Makaburi ya Rusororo katika mji mkuu Kigali, baada ya misa ya mahitaji ya mwanariadha huyo wa zamani.
Mwili wa Hakizimana ulikuwa umesafirishwa hadi Rwanda Jumamosi iliyopita. Hakizimana, 36, alikuwa mwanariadha mstaafu wa Rwanda ambaye alishikilia rekodi ya kitaifa ya mbio za mita 3000 kuruka viunzi na maji. Mwaka jana, alitumia miezi kadhaa kumsaidia Kiptum kulenga rekodi ya dunia.
Uhusiano wao kama kocha na mwanariadha ulianza mnamo 2018, lakini wenzi hao walikutana mara ya kwanza wakati mmiliki wa rekodi ya ulimwengu alikuwa mchanga zaidi.