Kocha wa FC Barcelona Xavi Hernandez ameshindwa kusafiri na timu yake kuelekea Marekani walikoenda Jumamosi kuweka kambi ya maandalizi ya msimu 2022/2023, huku Barcelona wakisema ni sababu za kiutawala na passport yake.
Xavi amekutana na changamoto hiyo ya visa na magazeti ya AS na Mundo Deportivo yamesema sababu ni kuwa na rekodi ya Xavi ya kuingia nchini Iran mara tatu ndio imemfanya azuiwe kiasi cha kuhitajika nyaraka zaidi za utetezi.
Marekani walitangaza kwa mtu atakayekuwa ameingia/kwenda Iran mara tatu au zaidi katika kipindi cha miaka 5 hatoruhusiwa kuingia Marekani isipokuwa kwa kibali maalum, hiyo inatokana na kuwa USA na Iran kutokuwa na mahusiano mazuri ya Kidiplomasia kiasi cha Iran kushukiwa kusapoti makundi ya kigaidi.
Xavi amewahi kwenda Iran mara tatu tofauti wakati akiitumikia wa Al-Sadd ya Qatar (2015-2021), Barcelona wamesema ataungana na timu Miami siku chache zijazo kwa ajili ya tour yao na kucheza mechi za kirafiki na Real Madrid, Inter Miami, Juventus na New York Red Bulls.