Korea Kaskazini siku ya Alhamisi ilikemea “chokozi za kizembe” zinazofanywa na Marekani na washirika wake kwa kukosoa uungaji mkono wa Pyongyang kwa vita vya Urusi nchini Ukraine, ikiwa ni pamoja na kutumwa kwa wanajeshi.
Katika taarifa iliyobebwa na Shirika rasmi la Habari la Korea, msemaji wa wizara ya mambo ya nje alisema mataifa 10 na Umoja wa Ulaya (EU) “yanapotosha na kukashifu” uhusiano wa “ushirika wa kawaida” wa Pyongyang na Moscow.
Pyongyang imetuma maelfu ya wanajeshi ili kuimarisha juhudi za vita vya Urusi, ikiwa ni pamoja na eneo la mpaka la Kursk, ambako vikosi vya Ukraine viliteka eneo hilo mapema mwaka huu.
Siku ya Jumatatu, mataifa hayo na Umoja wa Ulaya walisema kuongezeka kwa ushiriki wa Korea Kaskazini katika vita vya Ukraine katika kuunga mkono Urusi ni “upanuzi hatari wa mzozo huo, na madhara makubwa kwa usalama wa Ulaya na Indo-Pacific”.
Mawaziri wa mambo ya nje wa Australia, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan, Korea Kusini, New Zealand, Uingereza, Marekani na mwakilishi mkuu wa Umoja wa Ulaya walitia saini taarifa hiyo iliyotolewa na Washington.