Serikali ya Korea Kusini imetoa msaada wa vifaa mbalimbali venye thamani ya zaidi ya Bilioni moja kwa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) kwa ajili ya kuboresha Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa maarufu Sabasaba.
Vifaa hivyo vilivyotolewa na nchi hiyo kupitia Taasisi yake ya Biashara Korea Kusini (KOTRA) ni vibanda vya kisasa 500, kompyuta za mikononi 10, kompyuta za mezani (Disktop) 30, skana 30 pamoja na genereta lenye ukubwa wa Kv 60.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana mara baada ya kupokea msaada huo, Mkurugenzi Mkuu wa Tantrade, Latifa Khamis alisema vibanda hivyo vilivyotolewa vitaongeza ufanisi, mapato kwa nchi pamoja na idadi ya wadau mbalimbali kutoka mikoani kushiriki katika maonesho hayo ya Kimataifa ya Sabasaba.
“Msaada huu hauna masharti yeyote, hata hivyo wadau wengi walikuwa wanataka kushiriki maonesho lakini nafasi zilikuwa hakuna, lakini kupitia kuwepo kwa vibanda hivi tutaongeza ufanisi na idadi ya washiriki hatimaye kupata fedha zitakazoendelea kukuza uchumi wa nchi.
“Wadau wetu tunapenda kuwakaribisha kuja kwa wingi kwani uwezo wetu umeongezeka kutokana na kuwepo kwa vifaa hivi hivyo kwa mwaka huu maonesho yataimarika na kuwa yenye mvuto mkubwa,” alisema Latifa
Aidha alisema yapo mazungumzo ambayo wanayafanya baina yao na Kotra ambayo yanalenga kuboresha utendaji kazi ili kuweza kuwavutia zaidi wafanyabiashara.
Naye Balozi wa Korea Kusini nchini Tanzania, Kim Sun Pyo alisema ni muhimu kuendelea kuwahimiza watanzania kusafirisha zaidi bidhaa kwenda kuuza Korea na wao watawahamasisha wananchi wa Korea kununua bidhaa hizo.
“Tunahitaji kuhamasisha uhusiano wa pande zote mbili, tunao wajibu wa kuwahimiza watanzania kusafirisha bidhaa na kuzipeleka Korea kwa ajili ya kuziuza na tuwahamasishe wananchi wa Korea kununua bidhaa zinazotoka Tanzania,” alisema Pyo.Korea Kusini watoa msaada wa vifaa vya zaidi ya Bilioni moja kwa Tantrade