Mji mkuu wa DRC, Kinshasa, unabeba mzigo mkubwa wa kutokuwepo kwa mabasi kutoka kwa kampuni ya usafiri wa umma (Transco).
Kufuatia tatizo la ugavi wa mafuta wa serikali, kampuni inayosafirisha wakazi wa Kinshasa kwa bei nafuu inatatizika kwa shughuli ya usafirishaji wa watu. Suala hilo lilijadiliwa wikendi iliyopita wakati wa kikao cha baraza la mawaziri, lakini mgogoro huo bado haujatatuliwa.
Wateja walipata madhara siku ya Jumatatu huku msururu wa watoto wa shulewakiwa wanasubiri mabasi ya kampuni hiyo ilionekana kwenye barabara za mji mkuu asubuhi, huku watumishi wa umma wakijazana kwenye mabasi ya watu binafsi .
Hali hiyo ni neema kwa waendesha pikipiki za kukodiwa ambazo zimenufaika kwa kuongeza maradufu bei ya nauli.
Kampuni ya Transco inakosa mafuta kwa mabasi yake, lakini matatizo ni magumu zaidi. Serikali inatarajiwa kulipa karibu dola milioni 1 kila mwezi kwa kampuni kama ruzuku ya mafuta na vipuri.