Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imeingia makubaliano maalum na Benki ya NBC yanayohusisha ufadhili wa benki hiyo katika ujenzi na ukarabati wa kumbi kubwa za kisasa kwenye Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam ‘Sabasaba’ sambamba na ujenzi wa sanamu ya Rais wa Awamu ya tano Hayati John Pombe Magufuli.
Wakizungumza wakati wa hafla fupi ya kusaini hati ya makubaliano (MoU) yenye jumla ya thamani ya Tsh mil 420 jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade Balozi Mteule Edwin Rutageruka pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi walisema hatua hiyo inalenga kuleta mapinduzi makubwa kwenye Maonesho hayo yanayoendelea jijini humo huku yakivutia maelfu ya washiriki kutoka ndani na nje ya nchi.
Balozi Mteule Rutagaruka alisema mkataba huo unahusisha kipindi cha miaka mitatu huku akitaja maeneo yatayaoguswa na ufadhili wa benki hiyo kuwa ni pamoja na ukarabati mkubwa wa ukumbi unaofahamika kwa jina ‘Sabasaba’ wenye ukubwa wa mita za mraba 1600 ili uweze kuwa na hadhi ya juu zaidi si tu katika maonesho hayo bali pia katika wilaya yote ya Temeke.
“Kwa jitihada hizi za Benki ya NBC, kwasasa ukumbi huu ambao pia unatumika kama banda la maonesho ndio linalovutia zaidi washiriki wa kimataifa na limebeba hadhi hiyo ya kimataifa na ndipo yanapofanyika maonesho ya madini. Zaidi pia linatumika kamba kumbi ya mikutano ya kisiasa na shughuli za kijamii zikiwemo harusi,’’ Balozi Mteule Rutagaruka
Alitaja kumbi nyingine zitakazohusishwa na ufadhili huo kuwa ni pamoja na ukumbi wa Mikutano wa Rashid Mfaume Kawawa unaofanyiwa ukarabati mkubwa sambamba na ukarabati wa banda la bidhaa za viwanda vya Tanzania ambao utakarabatiwa katika hatua ya pili ya utekelezaji wa makubaliano hayo.
“Haya yote yanadhihirisha namna benki ya NBC inavyoshiriki katika kuchochea mazingira bora ya ufanyaji biashara,’’ alisema Balozi Mteule Rutagaruka huku akitolea mfano wa uwepo wa Kliniki ya biashara inayofadhiliwa na benki katika maonesho hayo ikihusisha uwepo wa taasisi na mamlaka mbalimbali za kibiashara ikiwemo Tantrade, Shirika la Viwango nchini(TBS), Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).
Kwa upande wake Sabi alisema ni heshima kubwa kwa benki hiyo kuingia katika ushirikiano huo kwa kuwa utatoa fursa kwao kufanikisha adhima ya msingi ya kuendelea kuwahudumia wadau wake muhimu wakiwemo wafanyabiashara wanaoshiriki maonesho hayo.
“NBC tumekuwa na utamaduni wa kuhakikisha kwamba ushirikiano wetu na wadau wetu haushii kwenye viunga vya majengo yetu au huduma tunazotoa kwao bali pia tumekuwa tukihakikisha kwamba tunakuwa nao bega kwa bega katika kurahisisha shughuli zao ikiwemo kuona kwamba wanafanya shughuli zao katika mazingira bora na ndio sababu tunakarabati hadi maeneo ya wao kufanya maonesho ya biashara zao huku pia tukiwasogezea huduma zetu za kifedha,’’ Sabi
Kuhusu ujenzi wa Sanamu ya Rais wa Awamu ya tano Hayati John Pombe Magufuli Sabi alisema unalenga kukumbuka jitihada na mchango wake katika kuinua uchumi wa viwanda nchini ambao ni kichocheo kikubwa cha biashara na ndio msingi wa maonesho hayo.