Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema hakuna mtu yeyote anayelidai Bunge akisisitiza kuwa orodha ya madai iliyosambaa mitandaoni ni ya mwaka 2018.
Ameeleza hayo bungeni mjini Dodoma kuhusu suala hilo aliloliita kuwa ni upotoshaji unaolenga kulivuruga Bunge.
Kwa mujibu wa Ndugai kuna orodha ya majina inayozunguka kwenye mitandao ya kijamii ikidai kuna watu wanalidai Bunge na baadhi ya majina yaliyomo kwenye orodha hiyo ni la mbunge wa zamani wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.
Kiongozi huyo amesema tangu kutolewa kwa tangazo hilo kwenye mitandao ya kijamii, simu yake imejaa jumbe wa waliokuwa wabunge katika Bunge la 11 wakimuleleza kuwa wanamdai.
“Kuna watu walipomaliza ubunge maisha yao ni magumu kweli, sasa anasikia kuwa anadai yaani ni tabu tupu, acheni, acheni jamani siyo kweli,” Ndugai.
Spika amesema wabunge wote walilipwa stahiki zao akiwemo aliyepo ng’ambo ambaye hakumtaja jina ambaye alidai kuwa alipoingiziwa fedha benki zilichukuliwa zote kwa sababu alikuwa anadaiwa.