Kundi la mataifa 7 tajiri duniani (G7) linatazamiwa kukubaliana juu ya kuanzisha mpango mpya wa kusambaza chanjo kwa nchi zinazoendelea katika mkutano wa viongozi wa wiki ijayo, gazeti la Yomiuri la Japan lilisema Jumamosi.
Mbali na G7, mataifa ya G20 kama vile India na mashirika ya kimataifa kama vile Shirika la Afya Duniani (WHO) na Benki ya Dunia yatashiriki, iliongeza, ikinukuu vyanzo vya serikali ya Japan.
Wakati wa janga la COVID-19, kituo cha COVAX, kikisaidiwa na WHO na Muungano wa Kimataifa wa Chanjo (GAVI), kilipeleka karibu dozi bilioni 2 za chanjo ya corona kwa nchi 146.
Hata hivyo, COVAX ilikabiliana na vikwazo katika kuhakikisha upatikanaji sawa wa chanjo kwani mataifa tajiri yalitanguliza chanjo kwanza kwa raia wao wakati wa uhaba wa maeneo ya kuhifadhi chanjo hizo katika mataifa maskini ulisababisha uchelewsho kwa usambazaji wa mamilioni ya dozi zilizokaribia kuisha muda.
Mpango huo mpya unalenga kukusanya fedha za siku za shida kwa ajili ya uzalishaji na ununuzi wa chanjo, pamoja na uwekezaji katika kutengeneza vifaa vya kuweza kuhifadhi chanjo na kuwapatia mafunzo wahudumu wa afya ili kujiandaa kwa janga lijalo la kimataifa, Yomiuri ilisema.
Chanzo:VOA