Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema nyakati za usiku katika mikoa 13 na kisiwani Zanzibar kumekuwa na hali ya joto kutokana na uwepo kwa kiwango kikubwa cha unyevu angani kinachofikia zaidi ya asilimia 80.
Hayo yameelezwa na mtaalamu wa hali ya hewa, Rose Senyangwa na kwamba vipindi hivyo vya joto vinatarajiwa kuongezeka Februari 2021.
Mikoa itakayokumbwa na joto ni DSM, Tanga, Pwani, Kaskazini mwa Morogoro, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Kagera, Mwanza, Geita, Shinyanga, Simiyu na Mara pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.
Senyangwa amesema ongezeko hilo la joto nchini limesababisha baadhi ya maeneo kuwa na unyevunyevu
“Tanzania vipindi vya jua la utosi hufika kilele kati ya mwishoni mwa mwezi Novemba wakati jua la utosi likiwa linaelekea kusini na hali hiyo hujirudia Februari wakati jua la utosi likielekea Kaskazini” Senyangwa
“Jua la utosi linaambatana na hali ya joto kali kwa sababu kipindi hicho ndipo uso wa dunia katika eneo tajwa huwa karibu zaidi na dunia kuliko maeneo mengine,” Senyangwa.
Senyangwa amesema katika kipindi cha Desemba, 2020 upungufu wa mvua unatarajiwa kujitokeza katika baadhi ya maeneo yanayopata mvua za vuli.
Ameyataja maeneo yatakayopata upungufu huo kuwa ni ukanda wa Ziwa Victoria, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki pamoja na Pwani ya Kaskazini na kwamba hali hiyo itasababisha kuwepo kwa hali ya joto.
Amesema hali ya joto inatarajiwa kupungua kidogo katika kipindi cha Januari 2021 kutokana na mvua zinazotarajiwa katika baadhi ya maeneo.