Tamasha la chakula la Coca-Cola Tanzania maarafu kama ‘Coca-Cola Food Fest’ limezidi kunoga huku muuzaji mmoja, maarufu “Baba Lishe,” akiibuka kuwa kivutio cha kipekee. Stanlaus Baron, ambaye ni muuzaji wa chakula anayekua kwa kasi, amejitokeza kupinga mitazamo ya kijinsia inayokita mizizi katika tasnia ya upishi, akionyesha kuwa jiko si la wanawake pekee.
Baron amepata umaarufu kupitia chakula chake chenye ladha ya kipekee cha tambi na maini huku mwenyewe akipinga wazo la kwamba upishi ni kazi ya wanawake pekee. “Kupika ni kipaji kama kazi nyingine yoyote,” alisema Baron alipokuwa akihojiwa huku wateja wakiendelea kufurika kwenye banda lake.
Tamasha la Chakula la Coca-Cola Tanzania limekuwa jukwaa muhimu la kuonyesha vipaji vya upishi kwa wilaya ya Kinondoni wiki hii baada ya kutembelea wilaya ya Ubungo wiki iliyopita, huku likileta pamoja wachuuzi wa chakula kutoka sehemu mbalimbali. Hata hivyo, hadithi ya Baron imechukua umaarufu wa kipekee, ikilenga kuvunja dhana potofu za kijinsia zilizodumu kwa muda mrefu ndani ya jamii ya Kitanzania.
Baron, ambaye alikua akivutiwa na upishi tangu utotoni, anasema alikumbana na upinzani kutoka kwa jamii na hata familia yake kwa sababu alikuwa mwanaume aliyeonyesha mapenzi makubwa kwa upishi. “Watu walikuwa wakiniambia kupika ni kazi ya wanawake, lakini sikukubaliana na hayo mawazo. Kupika ni ustadi muhimu, na furaha ya kuwahudumia watu kwa chakula kitamu haifananishwi na kitu chochote,” alisema.
Akiwa katika tamasha hilo, Baron alitoa wito kwa wazazi na walezi kote nchini kuacha kuwabagua watoto wao kwa misingi ya kijinsia, hasa linapokuja suala la vipaji vyao. Aliwataka wazazi kuwaunga mkono watoto wao, iwe ni katika upishi, uhandisi, au hata michezo. “Tunahitaji kuwapa watoto uhuru wa kufuata ndoto zao bila hofu ya kuhukumiwa,” aliongeza.
Kupitia mapokezi mazuri aliyopata kwenye tamasha hilo, Baron sasa ana mipango ya kupanua biashara yake, akiwa na ndoto ya kufungua mgahawa wake mwenyewe. “Hii ni mwanzo tu. Nataka kuendelea kuthibitisha kwamba yeyote, bila kujali jinsia, anaweza kufanikiwa jikoni,” alisema kwa kujiamini.
Ujumbe wa Baron unaonekana kuleta mabadiliko, sio tu katika tasnia ya upishi, bali pia katika jamii kwa ujumla. Katika tamasha ambalo limekuwa likitangaza vipaji vya upishi, hadithi ya Baron imeibuka kuwa moja ya za kukumbukwa zaidi mwaka huu, ikiashiria kuwa wakati mwingine, ujasiri na dhamira ndiyo viungo muhimu zaidi katika safari ya mafanikio.