Katika taarifa yake UN imetoa wito kwa kusitishwa kwa mauaji na ghasia na ukiukaji wa haki za binadamu.
Hali ya wasiwasi iliaanza tena kushuhudiwa kaskazini mwa taifa hilo baada ya kusitishwa kwa mapigano mengine katika jimbo jirani la Tigray, mapigano yaliohusishwa pia wapiganaji kutoka katika jimbo la Amhara.
Msemaji wa ofisi ya haki za kibinadamu ya umoja wa mataifa Marta Hurtado aliwaambia waandishi wa habari mjini Geneva kuwa wanasikitishwa sana na kuzorota kwa hali ya haki za binadamu katika baadhi ya mikoa ya Ethiopia.
UN imeeleza kuguswa zaidi na kinachoendelea katika eneo la Amhara, kufuatia kuongezeka kwa mapigano kati ya jeshi la Ethiopia na wanamgambo wa kikanda wa Fano hali iliyopelekea kutangazwa kwa hali ya dharura mnamo Agosti 4.
Mnamo Aprili serikali ya shirikisho ilitangaza kuwa imevunja vikosi vya mkoa kote nchini.
Hatua hiyo ilizua maandamano kutoka kwa wakaazi wa Amhara ambao walisema itadhoofisha eneo lao.
Mapigano yalizuka mapema mwezi Julai kati ya jeshi la taifa na wapiganaji wa eneo hilo wanaojulikana kama Fano, na kusababisha mamlaka mjini Addis Ababa mnamo Agosti 4 kutangaza hali ya dharura ya miezi sita.
Source: RFi