Ripoti iliyochapishwa Mei 10 na Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF)ikishirikisha wadau wengine inajadili kwa kina kuhusu uwepo wa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati yaani njiti.
Kwa ujumla, inasema kuwa viwango vya watoto kuzaliwa kabla ya wakati havijabadilika katika eneo lolote duniani katika muongo mmoja uliopita.
Kuzaliwa kabla ya wakati sasa ndio sababu kuu ya vifo vya watoto, ikichukua zaidi ya kifo kimoja kati ya vifo 5 vya watoto vinavyotokea kabla ya kutimiza umri wa miaka mitano baada ya kuzaliwa.
Watoto njiti wanaonusurika wanaweza kukabiliwa na changamoto ya afya ya maisha yote, pamoja na kuongezeka kwa uwezekano wa ulemavu na ucheleweshaji wa maendeleo.
Kutokana na ripoti ya mwaka 2012 kuhusu suala hili, ripoti hii mpya inatoa muhtasari wa kina wa kuenea kwa kuzaliwa kabla ya wakati na athari zake kwa wanawake, familia, jamii na uchumi.
Mara nyingi, eneo ambako watoto huzaliwa huamua ikiwa wataishi au la. Kusini mwa Asia na Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara ndiyo maeneo yaliyo na viwango vya juu zaidi vya watoto kuzaliwa kabla ya wakati, na watoto wachanga katika maeneo hayo wanakabiliwa na hatari kubwa zaidi ya vifo.
Kwa pamoja, maeneo hayo mawili yanachangia zaidi ya asilimia 65 ya watoto wanaozaliwa njiti. Ripoti hiyo pia inaangazia kwamba athari za migogoro, mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira, COVID-19, pamoja na kupanda kwa gharama za maisha kunaongeza hatari kwa wanawake na watoto.
Ripoti hiyo imebaini kuwa, muongo uliopita umeshuhudia uhamasishaji wa jamii kuhusu uzazi wa kujifungua kabla ya wakati na uzuiaji wa mtoto kufia tumboni, ukiendeshwa na mitandao ya wazazi na wataalamu wa afya.
Ripoti hiyo imesisitiza haja ya kuhamasisha rasilimali za kimataifa na za ndani ili kuboresha afya ya uzazi na watoto wachanga, kuhakikisha uangalizi wa hali ya juu unatolewa wakati na pale unapohitajika.