Katika Uchaguzi wa hivi karibuni Nchini Marekani, Wanawake weusi wameandika historia kwa kushinda viti viwili vya Seneti kwa mara ya kwanza ambao ni Lisa Blunt Rochester kutoka Delaware pamoja na Angela Alsobrooks kutoka Maryland wakishinda katika mbio zao na kuongeza idadi ya Wanawake weusi waliowahi kuchaguliwa katika Seneti kutoka wawili hadi wanne.
Huu ni ushindi muhimu ambao unaongeza uwakilishi wa Wanawake Weusi katika siasa Nchini Marekani.
Blunt Rochester amekuwa Mwanamke wa kwanza na mweusi kuwakilisha Jimbo la Delaware katika Seneti, wakati Alsobrooks akiwa Mwanamke mweusi wa kwanza kuwakilisha Jimbo la Maryland ambapo kupitia ushindi huu umeongeza idadi ya Wabunge weusi katika Seneti hadi watano ikiwa idadi kubwa zaidi kuwahi kutokea katika historia ya Seneti ya Marekani.
Kwa mujibu wa Kelly Dittmar, Mkurugenzi wa utafiti katika Kituo cha Wanawake wa Marekani cha Chuo Kikuu cha Rutgers, ushindi huu ni hatua nzuri ya kuonyesha ongezeko la uwakilishi wa Wanawake katika siasa lakini pia unatoa tahadhari kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanyika ili kufikia uwakilishaji sawa pia anasisitiza kuwa Wanawake wa Marekani hasa Wanawake wenye asili ya Kiafrika, hispania, Waasia na Wahindi bado hawawakilishiwi sawasawa katika Ofisi za Uchaguzi.
Ikiwa ushindi wa Blunt Rochester na Alsobrooks umeongeza uwepo wa Wanawake weusi katika Seneti ya Marekani bado Seneti inaendelea kuwa na uwakilishi mdogo wa Wanawake na Watu wa rangi nyingine, huku ikiwa na asilimia kubwa ya Wanaume weupe.
Hata hivyo ushindi huu unaonyesha mabadiliko katika mfumo wa kisiasa na umuhimu wa Wanawake weusi kuwa sehemu muhimu ya siasa ya Marekani.