Mamlaka za Palestina zimetangaza kuwa, jeshi vamizi la utawala wa Kizayuni wa Israel limeua watoto 11,000 na wanawake 7,500 katika Ukanda wa Gaza na kuongeza kuwa jeshi hilo katili limedondosha zaidi ya tani 65,000 za mada za miripuko katika vita vya upande mmoja lilivyoanzisha dhidi ya Wapalestina waliowekewa mzingiro.
Taarifa hiyo iliyotolewa jana Jumatatu imeendelea kueleza kuwa, Wapalestina wapato 7,000 – asilimia 70 kati yao wakiwa ni wanawake na watoto – bado wako chini ya vifusi au wamepotea kutokana na mashambulizi ya kiholela ya jeshi la Israel.
Takwimu zinazoakisi ukubwa wa jinai na mauaji yaliyofanywa na jeshi la Kizayuni katika Ukanda wa Gaza zinaonyesha pia kwamba, mashambulio ya jeshi hilo yamebomoa kikamilifu nyumba zipatazo 70,000 na kuzifanya zingine 290,000 zisiweze kukalika vita vyake vya siku 108 dhidi ya Wapalestina wasio na ulinzi.
Kuhusu mashambulizi ya jeshi la Kizayuni kwenye sekta ya afya, Mamlaka za Palestina katika Ukanda wa Gaza zimeeleza kuwa jeshi hilo hadi sasa limeshawaua wafanyakazi 337 wa kada ya afya na tiba na maafisa 45 wa ulinzi wa raia.
Halikadhalika, tangu Oktoba 7,2023 jumla ya waandishi wa habari 119 wameuawa katika mashambulizi ya kiholela yaliyofanywa na jeshi la Israel.