Gwiji kutoka nchini Tanzania, Lady Jaydee, anayejulikana pia kama ‘Malkia wa Bongo Flava’ amesaini mkataba wa usambazaji na kampuni ya Universal Music Group East Africa (UMG EA). Yote yanajiri mwezi mmoja baada ya kutambulishwa kwenye jukwaa la Bongo Flava Honors kwa mchango wake mkubwa katika ukuaji wa muziki wa Bongo Flava nchini Tanzania.
Dili hilo linaenda sambamba na Lady Jaydee kusherehekea miaka 25 kwenye tasnia ya muziki. Baada ya kudumu katika game ya muziki nchini Tanzania na kutambuliza kama ‘Komando Jidee’ anafuraha kusherehekea mafanikio haya kwa kutia saini mkataba na UMG Afrika Mashariki.
Mkataba huo unathibitisha kuongezeka kwa wasanii orodha ya UMG EA katika Afrika Mashariki na kuonyesha umahiri wa Lady JayDee kama nguzo ya muziki katika eneo hilo.
Lady JayDee alizaliwa na kupewa jina Judith Mbibo mwaka 1979 kisha safari yake ya muziki ilianza mwaka 1990. Alianza kama rapper kisha baadae akapata njia mpya ambapo sauti yake ilivuma kwa kasi. Ukuwaji wa jina lake umejengwa kutokana na utunzi wa muziki wa kipekee huku muziki huo ukipaza sauti nguvu na uwezo wa mtoto wa kike katika tasnia ikifanya talanta hii kupokelewa kwa upendo na kuungwa mkono na mashabiki kutoka nchini Tanzania, Kenya na nchi zingine za Ukanda wa Afrika Mashariki.
Akiwa na albamu 9 na zaidi ya tuzo thelathini za ndani na nje ya nchi kwa jina lake, Lady Jaydee amekuwa mwanamapinduzi katika kuboresha muziki wa Bongo Flava kupitia kuachia muziki, kuzunguka na kufanya maonyesho mbalimbali nchini Tanzania, barani Afrika na duniani kote, huku akishiriki kwa kuwa mmoja wa majaji katika show za televisheni kama “The Voice Africa”
Kwa kuongezeka kwa wasanii katika orodha ya vipaji Afrika Mashariki, UMG EA imetoa fursa ya kuleta mwanga mpya katika ukanda huu na kusafirisha vipaji katika safu za kimataifa.
Lady Jaydee aingia kwenye orodha ya wasanii wa UMG tayari kuchagiza tasnia hiyo zaidi.
Universal Music Group (UMG) ni kampuni inayoongoza ulimwenguni katika kuleta burudani ya muziki, ikiwa na safu pana ya biashara zinazojishughulisha na muziki uliorekodiwa, uchapishaji wa muziki, uuzaji na maudhui ya sauti inayoendeshwa ndani ya zaidi ya nchi 60 duniani.
Ikijumuisha orodha za rekodi za muziki na nyimbo za kila aina, UMG hutambua na kukuza wasanii, kuzalisha na kusambaza muziki unaosifiwa zaidi na uliofanikiwa kibiashara duniani.