Marekani imeweka vikwazo vipya vinavyolenga kuvuruga mkondo wa ufadhili wa Hamas baada ya mashambulizi yake mabaya nchini Israel.
Kundi la wanamgambo wa Kipalestina lina mtandao tata wa ufadhili ambao hutumia kutoa msaada kutoka kwa mashirika ya misaada na wafadhili wa kibinafsi, pamoja na mataifa rafiki kama vile Iran na Qatar.
Pesa hupitishwa kupitia mtandao wake wa chinichini wa handaki au kutumia fedha fiche ili kukwepa vikwazo vya kimataifa baada ya kuteuliwa kuwa shirika la kigaidi na Marekani na Umoja wa Ulaya.
Wizara ya mambo ya nje ya Marekani ilisema ina ushahidi kwamba Iran hutoa hadi $100m (£82.3m) kwa makundi ya Wapalestina ikiwa ni pamoja na Hamas kila mwaka.
Iran ilikanusha kuwa ilisaidia Hamas kushambulia Israel – ambayo haiitambui – lakini ilishangilia matokeo.
Hamas pia huongeza mapato kupitia ushuru wa mishahara, misaada, uagizaji bidhaa na shughuli nyingine za kiuchumi ndani ya Gaza.
Polisi wa Israel walisema hivi majuzi walifanya kazi na Uingereza kufungia akaunti ya benki ya Barclays iliyohusishwa na uchangishaji fedha kwa ajili ya Hamas, na pia wamefaulu kufungia akaunti za cryptocurrency zilizokuwa zikitumiwa na kundi hilo kuomba fedha.
Kampuni ya utafiti ya TRM Labs ilisema mamlaka ya Israeli imenasa “makumi ya mamilioni ya dola” kwa njia ya crypto kutoka kwa anwani zilizounganishwa na Hamas katika miaka ya hivi karibuni.