Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imetoa onyo la tahadhari kwa Kampuni ya New Force kutokana na kuwa na matukio mengi ya ajali ambapo imesema hali ya kuendelea kuwepo na matukio ya ajali kutokana na uzembe wa Madereva wa New Force haikubaliki.
LATRA imeitaka Kampuni hiyo kutafuta suluhisho la sababu za ajali hizo haraka na Mamlaka itaendelea kuifuatilia kampuni hiyo kwa ukaribu, vinginevyo Mamlaka haitasita kuchukua hatua zingine za kisheria ikiwa ni pamoja na kufuta leseni za usafirishaji za kampuni hiyo.
“Itakumbukwa kuwa mnamo tarehe 3 Julai, 2023 Mamlaka ilisitisha ratiba za mabasi 38 ya kampuni hiyo kuanza safari zake saa tisa (9:00) alfajiri na saa kumi na moja (11:00) alfajiri ikiwa ni sehemu ya hatua za kupunguza ajali za barabarani katika kampuni hiyo, adhabu hiyo ilitokana na kuwepo kwa mfululizo wa ajali katika kipindi cha wiki nne mfululizo, hata hivyo, kampuni hiyo imeendelea kuwa na matukio ya ajali”
“Tarehe 7 Agosti, 2023 basi Na. T618DMG lilipata ajali kati ya maeneo ya Ruahambuyuni na Mikumi na kama ilivyokuwa kwenye ajali nyingine, sababu ya ajali hii ilikuwa ni uzembe wa dereva kutaka kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari”